Jumatano, 12 Desemba 2012

UNAIJUA HII; SHULE YA KWANZA TANZANIA ILIJENGWA MUHEZA MKOANI TANGA!!!?

Shule ya kwanza Tanzania ilijengwa Muheza

Baadhi ya majengo yaliyojengwa shuleni hapo enzi hizo.
 
Na Elias Msuya 
MWAKA 1848, Mmishenari wa Kijerumani Dk Johan Ludwig Krapf,   alitembelea kijiji cha Magila kilichopo  Muheza mkoani Tanga akiwa katika safari zake za Afrika Mashariki.
Magila kuna  mlima ulio katika safu za milima ya Usambara ukipakana na mlima wa Magoroto ambao ndio  chanzo cha maji ya mto Mkurumuzi unaoelekea Muheza.
Historia inaonyesha  eneo la mlima   Magila wenye  miamba na mawe mengi, zamani kabla ya kuja wageni  lilitumika kuwatenga wagonjwa wa ukoma na magonjwa mengine yasiyotibika, kwa lengo la kuwazuia wasiwaambukize wengine.
Dk Krapf alipofika na kuwaona wagonjwa hao  waliokuwa wakiishi kwa madhila makubwa, alichonga msalaba katika mti wa mkuyu kwa imani kuwa Mwenyezi Mungu angewaponya wagonjwa hao.
Eneo hilo ndilo lililokuja kujengwa shule ya kwanza na Waingereza mwaka 1886. Alama ya msalaba huo ipo hadi na sasa na ndipo ilipo Shule ya Sekondari  Hegongo.
Hadi leo mahali hapo panaitwa Magila Msalabani. Kwa sasa Magila ni kata yenye vijiji vya vya Magila, Mikwamba, Misongeni na Mafleta.
Nilifika katika eneo hilo nilipokuwa wilayani Muheza hivi karibuni ili kuchunguza historia ya eneo hilo.
Hapo nikutana na Luteni Kanali mstaafu John Mhina ambaye amekamilisha kuandika kitabu kuhusu historia ya Magila Msalabani,  kinachoeleza historia ya kijiji hicho na ujio wa wazungu walioanzisha shule ya kwanza Tanganyika na kanisa.
Luteni Kanali Mhina aliyelitumikia Taifa kwa muda mrefu kama mwanajeshi , na baadaye kuwa Mbunge wa Muheza kutoka mwaka 1990 hadi 1995,  anasema harakati za kuanzisha shule katika kijiji hicho zilitokana na Wamishenari waliokuja Afrika Mashariki kutoka Ulaya kwaajili ya kueneza dini ya kikristo tangu miaka ya 1770.
Anawataja baadhi ya Wamishenari hao kuwa ni pamoja na David Livingstone, Charles Mackenzie, William Tozer na Edward Steer.
Anasema harakati hizo zilianzia tangu visiwa vya Zanzibar mwaka 1863 ambako pia walikomesha biashara ya utumwa na kuanza ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mkunazini Zanzibar kwa miaka 10 tangu mwaka 1873.
Anasema wakati huo kulikuwa na shule iliyoanzishwa Zanzibar maeneo ya Kiungani na Kiinua mguu na Askofu William Tozer mwaka 1869. Hata hivyo,  anasema shule hiyo haikuwa rasmi na ilikuwa ikifundisha elimu ya dini kwa watumwa waliokombolewa.
Credits; Gazeti laMwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni