Jumatano, 12 Desemba 2012

WATATU WAKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI HUKO IRINGA

Pembe za ndovu 


Pembe hizo zilizoelezwa kuwa zimetokana na tembo 39 wenye thamani ya Sh934.8 milioni, zilikamatwa juzi saa 12 jioni, baada ya gari lililokuwa na shehena ya mzigo huo kushtukiwa na askari waliokuwa katika Kituo cha Ukaguzi cha Igumbilo kilichopo Iringa Mjini.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema jana: “Watuhumiwa walikamatwa kutokana na kusita kusimamisha gari lao baada ya kushukiwa na askari. Haina shaka kwamba tembo hao waliuawa katika uwindaji haramu unaodaiwa kuendelea mkoani Mtwara,” alisema Kamanda Kamuhanda na kuongeza: “Askari walipolisimamisha gari hilo, dereva alijifanya anasimama, lakini baadaye akaanza kulikimbiza ndipo polisi walipoanza kulifukuza.”


Kamuhanda alisema kutokana na gari hilo kuwa na mwendo wa kasi kuliko la polisi, walilazimika kuchukua gari la msamaria mwema aina ya Toyota Land Cruiser na kuendelea kulikimbiza.“Wakati wanalifukuza gari hilo, askari waliwasiliana na polisi wa Kituo cha Ruaha Mbuyuni ambao waliweka kizuizi.”


Kamanda Kamhanda alisema baada ya kufika eneo hilo na kubaini kizuizi hicho, dereva wake aligeuza gari hilo kwa kasi na kuanza kurudi.


Alipofika mbele kidogo, watuhumiwa walilitelekeza na kukimbilia kichakani.Kitendo hicho kiliwavuta baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo na baada ya kufika hapo, walishirikiana na polisi kuingilia kichakani kuwasaka watu hao na kuwakamata muda mfupi baadaye.


Kamanda huyo alisema polisi waliokuwa wakilifuatilia gari hilo, walilipekua na kukuta pembe hizo zenye uzito wa kilo 211.6.
“Thamani ya pembe hizo ni Sh186,680,000. Lakini gharama za jumla kwa tembo 39 waliouawa ni Sh934,830,000,” alisema.


Kamanda Kamuhanda alisema mbali na kuwashikilia watu hao watatu, polisi inaendelea na kufanya uchunguzi ili kuwabaini wahusika zaidi wa uharamia huo.
“Tunaamini bado kuna watu nyuma yao, siyo rahisi hao waliokuwa wanasafirisha, kuwa ndiyo waliokuwa wamewawinda tembo hao,” alisema na kuongeza;


“Sisi tunaendelea na uchunguzi na utakapokamilika tutawafikisha watuhumiwa wote mahakamani. Si kweli kwamba hawa waliokuwa wakisafirisha ndiyo wameingia kwenye mbuga za wanyama na kuua wao wenyewe,” alisema.


Kamanda huyo alisema mbali na pembe hizo za ndovu, katika upekuzi huo, polisi walibaini aina mbili za namba za usajili wa gari lililokuwa limebeba shehena hiyo ya nyara za Serikali.
“Watuhumiwa walitumia namba mbili za gari. Wakati gari hilo linapita eneo la Igumbilo, lilikuwa na namba tofauti na zilizokutwa Ruaha. Hali hii ilifanya kazi ya kutambua gari kwa kutumia namba kuwa ngumu, lakini aina ya gari na rangi vilisaidia,” alisema

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni