Jumapili, 20 Oktoba 2013

UTATA WAGUBIKA MAUAJI YA MKE WA OFISA WA BOT.



Baadhi ya watu wakiwa kwenye chumba alichoingilia muuaji kama inavyoonekana juu. Picha na Editha Majura 
Inaelezwa kuwa mtu huyo aliingia kupitia sebuleni, Anna alisikia kishindo, alipotoka chumbani kwenda kuangalia ndipo akakutana na muuaji ambaye alimnyonga.
Hata hivyo kabla ya umauti, Anna alipiga kelele zilizosababisha baadhi ya majirani kuizingira nyumba. Kilio chake hakikuzuia asiuawe kwa vile hata majirani walishindwa kuingia kwa vile nyumba ilikuwa imefungwa; Muuaji aliendelea kumnyonga hadi kufa licha ya kuomba asiuawe.
Majirani waliosikia kilio cha kuomba msaada waliizingira nyumba hiyo wakihangaika namna ya kuingia ndani bila mafanikio, kwani milango yote ilikuwa imefungwa.
Baadaye walitoa taarifa polisi kupitia kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Malela, wakati askari wanafika Anna hakuwa anaendelea kupiga kelele za kuomba msaada, huku wengi wakifikiri labda amejificha au amekufa.
Polisi walipoingia walimkuta Anna kwenye korido, akiwa hajitambui, walipompeleka hospitali ndipo ikathibitika kwamba alikuwa amekufa.
Muuaji alikutwa amejificha chooni ndani ya nyumba hiyo, anasema Mkuu wa Upelelezi katika Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala, Thobias Walelo.
Polisi wakiri kweli elimu haina mwisho
Wahenga walisema ‘Elimu haina mwisho’. Usemi huu umethibitika kwa kamanda wa upelelezi wa Wilaya ya kipolisi Mbagala, mkoani Temeke, Jijini Dar es Salaam, Thobias Walelo wakati akizungumzia mauaji ya Anna Mbago (35).
“Unaposikiliza maelezo ya muuaji, ukizingatia mazingira ya tukio, siyo rahisi kuamini kilichotokea, nakiri tukio hili ni la aina yake kwangu, limenidhihirishia kuwa elimu haina mwisho, napaswa kuendelea kujifunza zaidi kama ambavyo wanadamu tunapaswa kuendelea kujifunza bila kuchoka hadi siku ya mwisho wa uhai wetu,”anaeleza ASP Walelo.
Mtuhumiwa akijieleza;
“Naitwa (jina tunalo), ninafanya biashara ya sigara, naishi Mbagala” anasema mtuhumiwa wa mauaji hayo akiwa mikononi mwa polisi
 Anasema Oktoba 10 mwaka huu, saa 4:00 asubuhi aliondoka nyumbani kwao, akitembea kwa miguu kwa lengo la kutafuta riziki.
“Nikafika sehemu nisiyoifahamu, nikasogelea nyumba moja na kuchungulia dirishani, nikaona mwanamke akihesabu fedha, zikanitamanisha na kuanza kutafuta jinsi ya kuingia ndani ya nyumba hiyo,”anaeleza mtu huyo ambaye, anasema hadi wakati anakamatwa hakuwa ameiba kiasi chochote cha fedha.
Anasema tukio hilo alilifanya saa 2: 00 usiku. Ni kwamba alipofika kwenye nyumba hiyo akagundua upande wa kulia wa nyumba hiyo, kwenye dari kumeachia kidogo, hivyo akazunguka upande wa mbele ya nyumba na kukwea kwenye kibaraza.
Akaambaa na ukuta mpaka eneo ambalo dari  ilionesha kuachia, akaipasua na kuingia ndani mpaka sebuleni. Anasema hapo pia alifumua dari na kudumbukia ndani kwa kutua kwenye moja ya sofa.
Anasema Anna alishtushwa na kishindo chake alipotua kwenye sofa, hata hivyo kwakuwa alishafunga milango, hakuweza kukimbilia nje zaidi ya kupiga kelele akiomba msaada.
“Nilimkimbilia na kumzuia asipige kelele lakini hakuacha, nikamkaba ili asiendelee kupiga kelele, tukapambana nikamshinda nguvu, nikamkaba mpaka alipoishiwa nguvu,” anaeleza mtuhumiwa huyo.
Credits; Gazeti la Mwananchi..