LAW/SHERIA

FROM NOW ONWARDS WE PROUDLY WANT TO INTRODUCE A NEW PAGE IN THIS COMMUNITY BLOG WHICH WILL ANALYSE SOME MATTERS ON THE LAW OF THE LAND AND SOMETIMES PUBLIC INTERNATIONAL LAWS, THE AIMS IS TO PUT PUBLIC AWARENESS ON THE SAME AND STAKEHOLDERS ARE INVITED TO ENLISH THE PAGE BY YOUR OPINIONS AND PRESENTATION. IT IS JUST THE START OF THE RACE FOR EXPECTED YOUNG BARRISTERS . YOU ARE WELCOME.                                                                                              



KATIBA NI NINI?
 Katiba ya nchi ni mkataba wa namna nchi itakavyoendeshwa ikizingatia masuala makuu ya msingi ikiwemo haki za raia,namna uongozi wa nchi utakavyopatikana, vipaumbele vya taifa mila na desturi za watu wa taifa husika. Mkataba huu ni kati ya wananchi na kikundi cha wananchi wachache walioteuliwa kuongoza wenzao.(viongozi)

Wananchi wanakubali kutoa madaraka ya kuongoza nchi yao kwa viongozi wao(serikali) ili watekeleze makubaliano yaliyomo ndani ya katiba kwa kufuata vigezo mbalimbali mfano serikari ikishindwa kuongoza vizuri basi itabidi iachie madaraka na wawekwe wengine watakaotekeleza mkataba ule.(katiba)

Hivyo basi watawaliwa wanajitoa na kukubali kukabidhi madaraka ya kuongozwa kwa kikundi kidogo cha watawala(dola) ambacho kina watu toka jamii ileile, ndio maana tunaita mkataba. Katiba ni sheria mama, mambo yote yatakayotekelezwa au sheria zitakazotungwa itabidi zifuate matakwa ya katiba ile, yasiwe kinyume. Mfano katiba ikisema; "Ardhi ni mali ya Rais wa Nchi, kila mwananchi ana haki ya kumiliki ardhi." Basi kusitokee itakayosema vinginevyo kama, Matajiri au mtu mmoja anaweza kumiliki ardhi kubwa na kuihodhi wakati wananchi wengine hawana hata kipande cha kulima bustani. nbsp;WARMLY WELCOME.



SHERIA YA MIRATHI YA TANZANIA

SHERIA YA USIMAMIZI WA MIRATHI SURA YA 352 YA SHERIA ZA TANZANIA

1. SHERIA HII INASHUGHULIKA NA MAMBO YAPI NA INA LENGO GANI HASA?

Lengo kuu la sheria hii ni kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu baada ya kifo chake ikiwamo kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa marehemu kwenda kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo.Nia hasa ni kwamba mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure,au warithi halali au watu wenye maslahi na mali za marehemu,kwa mfano wale wanaomdai hawapotezi haki hiyo, bali awepo mtu ambaye atazisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai na kuepusha mgongano katika jamii husika.Hivyo sheria inamuweka msimamizi wa kugawa mirathi husika na mamlaka yake.

2. MAHAKAMA ZIPI ZINA MAMLAKA YA KUSIKILIZA MASUALA HAYA
Mirathi inaweza kufunguliwa katika mahakama mbalimbali kutegemea na sheria itakayosimamia mirathi husika.

v Kama sheria ya kimila itatumika katika kugawa mirathi basi shauri la kuomba usimamizi wa mirathi litafunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo.Msimamizi wa mirathi anatakiwa airidhishe mahakama kwamba marehemu kutokana na maneno yake,mfumo wake wa maisha au maandishi aliyoacha,alionyesha nia kwamba mirathi yake alitaka iendeshwe kwa kufuata sheria za kimila.

v Kama sheria itakayotumika ni ya kiisilamu basi shauri la kuomba usimamizi wa mirathi litafunguliwa Mahakama ya Mwanzo.Msimamizi wa mirathi anatakiwa airidhishe mahakama kwamba marehemu kutokana na maneno yake,mfumo wake wa maisha au maandishi aliyoacha,alionyesha nia kwamba mirathi yake alitaka iendeshwe kwa kufuata sheria za kiislamu.


v Kama sheria itakayotumika kugawa mirathi ni ya Serikali basi mahakama wilaya,mahakama ya hakimu mkazi na mahakama kuu zinahusika kutegemea thamani ya mali alizoacha marehemu.

· Thamani ya mali yote aliyoiacha marehemu isiyoondosheka isiyozidi shilingi milioni 5 (Mfano nyumba, mashamba) na inayoondosheka isiyozidi shilingi milioni 3 (mfano magari) mirathi ya aina hii inafunguliwa Mahakama ya Mwanzo.
· Thamani ya mali yote aliyoiacha marehemu isiyohamishika isiyozidi shilingi milioni 12 na inayohamishika isiyozidi shilingi milioni 100 mirathi hii inafunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ama ya Hakimu Mkazi.
· Thamani ya mali inayozidi shs millioni 150 mirathi hii inafunguliwa mahakama Kuu.

3. SHERIA NA SIFA ZA KUWA WASIMAMIZI WA MIRATHI.

A] Ndugu wa marehemu na wale wenye maslahi na mirathi ya marehemu,kwa mfano wale ambao wanatarajia kupata sehemu ya mirathi ya marehemu.

B] Mtu au watu wanaomdai marehemu,Mtu huyu hufungua mirathi pale ambapo ndugu wa marehemu wameshindwa au hawataki kufungua mirathi.

C] Kkabidhi wasii mkuu, huyu au hii ni ofisi ya serikali ambayo hujihusisha,Pamoja na mambo mengine,usimamizi wa mirathi,endapo itaombwa na mtu yeyote.

D] Muwakilishi wa kisheria mtu aliyetajwa kama msimamizi wa mirathi [mtu aliyepewa power of attorney]

E]Mtu yeyote ambaye mahakama kwa kuangalia vigezo mbalimbali vikiwamo udugu,maslahi ya muhusika katika mirathi hiyo,usalama wa mali za mirathi pamoja na uwezekano wa kuisimamia vizuri,anaweza kuteuliwa na mahakama

VILEVILE Sheria imetoa baadhi ya vigezo ambavyo mtu lazima awe navyo ali apate usimamizi wa mirathi
I]awe mtu mzima
Ii]awe na akili timamu


4. KUNA NAMNA NGAPI ZA UTOAJI WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Namna ya kutoa usimamizi wa mirathi hutegemea jinsi marehemu alivyojiandaa kukutana na kifo chake,kuna wengine huacha wosia na wengine huwa hawaachi wosia.
A] KAMA KUNA WOSIA
Kama kuna wosia usimamizi wa mirathi hupewa mtu yule tu aliyetajwa kwenye wosia,mtu huyo anaweza kuwa ametajwa moja kwa moja au kwa hali halisi ilivyojionyesha kwenye wosia kwamba lazima atakuwa ni yeye.Hivyo kuandika wosia ni nafasi pekee ya kuchagua msimamizi wa mirathi.

Vile vile mtoa wosia anaweza kuchagua mtu zaidi ya mmoja kusimamia mirathi yake.Ikumbukwe kuwa kuna wosia za aina mbili.Ya kwanza ni wosia wa maandishi na wa pili ni ule wa maneno.Wosia wa maneno ni lazima uthibitishwe kwa ushahidi wa wahusika ambao ulitolewa mbele yao.Pale ambapo mahakama itajiridhisha na uwepo wa wosia na ikatoa amri ya usimamizi itakuwa imethibitisha usahihi wosia husika.Wosia wa maandishi nao lazima uthibitishwe angalau kwa kuleta mtu aliyeshuhudia ukiandikwa ili athibitishe kwamba marehemu alikuwa na akili timamu wakati akiandika wosia huo na hakulazimishwa na mtu yeyote.

B] WOSIA ULIOMBATANISHWA NA BARUA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Hii hutokea katika mazingira yafuatayo

i] Pale ambapo marehemu ameacha wosia lakini wosia huo haujamtaja mtu ambaye amarehemu alitaka awe msimamizi wa mirathi yake

ii] Pale ambapo watu wote waliotajwa na marehemu katika wosia kwamba wasimamie mirathi yake wamekataa hoja hiyo au ni watu ambao kisheria hawana uwezo wa kusimamia mirathi,kwa mfano mtoto,mtu asiye na akili timamu

iii] Pale ambapo wasimamizi wote wa mirathi walitajwa katika wosia wamefariki kabla mwandika wosia hajafariki au amefariki kabla ya kumaliza kazi yake ya usimamizi wa mirathi.
Katika hali kama hii,lazima ndugu wakae wachague mtu ambaye wamempendekeza kuwa msimamizi wa mirathi na watatakiwa waende mahakamani na wosia huo ili wakaombe mahakama imthibitishe rasmi.Hapa ndipo amri ya usimamizi wa mirathi ukiwa na wosia ulioambatanishwa na barua ya usimamizi wa mirathi hutolewa.

C] KAMA HAKUNA WOSIA
Kama marehemu hakuacha wosia wowote,barua za usimamizi wa mirathi zinaweza kutolewa kwa mtu yoyote ambaye kwa mujibu wa taratibu za usimamizi wa mirathi zinazohusika katika mirathi hiyo[za kimila au za kiserikali au za kiislamu] atakuwa ana haki ya kupata mali zote za marehemu au sehemu ya mali hizo.Pale inapotokea mtu zaidi ya mmoja ameomba usimamizi wa mirathi ya marehemu,mahakama itakuwa na utashi wa kuchagua mmoja au mtu zaidi ya mmoja kusimamia mali za marehemu,na katika kufanya hivyo mahakama inatakiwa kisheria iangalie mtu mwenye maslahi makubwa zaidi naya karibu na mirathi hiyo kuliko yule mwenye maslahi madogo.Vile vile kama itatokea kwamba marehemu alikuwa anadaiwa,na hakuna ndugu aliyefungua mirathi ya marehemu mahakamani,basi mdai ana uwezo wa kuomba kufungua mirathi husika
Mahakama inapoona kwamba ni muhimu au ni busara kumchagua mtu ambaye katika hali ya kawaida asingechaguliwa kusimamia mirathi,mahakama,kwa kuangalia ukaribu wa kiundugu,maslahi aliyonayo muhusika katika mirathi,usalama wa mirathi husika na uwezekano wa mirathi hiyo kusimamiwa vyema,itamchagua mtu huyo asimamie mirathi.


D] USIMAMIZI WA MIRATHI KWA MAMBO MAALUMU.
I] USIMAMIZI WA MIRATHI WAKATI SHAURI LIKIENDELEA KUSIKILIZWA
Inawezekana kwamba
-bado kuna ubishi mahakamani kuhusu uhalali wa wosia,au
shauri la kuomba kupata barua ya usimamizi wa mirathi kwa mtu ambaye hakuacha wosia bado linaendelea au
-shauri la kuomba mahakama izifute barua za usimamizi wa mirathi alizopewa mtu Fulani linaendelea ,
-mahakama ina uwezo wa kuteua msimamizi wa muda wa mali za marehemu huku kesi ikiendelea mahakamani.Msimamizi huyu atakuwa na mamlaka kamili kama aliyo nayo msimamizi ma kudumu wa mali za marehemu isipokuwa tu haruhusiwi kugawanya mali za marehemu.Vilevile msimamizi huyu atakuwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa mahakama. Ili muhusika apate ruksa hii ni lazima atoe sababu za kuonesha dharura ya ombi husika na umuhimu wakeSuala hili limekuwa likiwatatiza hasa hasa akina mama na watoto.Inaweza kutokea watoto bado wanasoma shule na baba yao akafariki.Baba ana mali nyingi pengine ana akaunti benki.Lakini pengine ndugu au watu wowote bado wanabishana mahakamani kwamba ni nani ana haki ya kusimamia mirathi.Ni mara nyingi inatokea mahakama inaruhusu akina mama hawa kuchukua kiasi Fulani cha pesa kulipa ada za watoto wao,kuwatibu,hata matumizi ya muhimu ya nyumbani bora tu wasijihusishe na kugawa mali za marehemu.


ii] MTEULIWA WA KUSIMAMIA MIRATHI BADO ANA UMRI MDOGO

Pale ambapo mtu anayatakiwa kusimamia mirathi bado ana umri mdogo,usimamizi wa muda hupewa mtu mzima ambaye atakuwa ameteuliwa na mahakama kama mwangalizi wa mtoto na mali zake au kwa mtu yeyote ambaye mahakama itaona anafaa mpaka pale muhusika atakapokuwa mtu mzima na kuwa na uwezo wa kusimamia mali zake vizuri.

Iii] MTEULIWA WA KUSIMAMIA MIRATHI HANA AKILI TIMAMU
Pale ambapo mtu anayetarajiwa kusimamia mirathi hana akili timamu,mahakama itamteua mtu ambaye atasimamia mirathi hiyo kwa muda na kwa faida ya muhusika mpaka pale atakapokuwa na uwezowa kiakili wa kuisimamia mirathi husika

Iii] USIMAMIZI WA MIRATHI KWA AJILI YA KUKUSANYA NA KUTUNZA MALI ZA MAREHEMU
Kama inaonekana ni muhimu kwamba mali za marehemu zikusanywe na kuhifadhiwa pahal pamoja,mahakama inaweza kutoa usimamizi huo kwa mtu yoyote ambaye anafaa ili afanye kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kulipa madeni lakini haruhusiwi kugawa mali kwa warithi